SAYARI YA JUMATANO MERCURY-ATTARID
Sayari hii iko Mbingu ya 2, Malaika wake Mikyaail au Raphael. Jini anayetawala Jumatano anaitwa Barkaan au Ophiel,
Siku zake ni Jumatano na Jumamosi usiku na Nyota zake ni Mapacha na Mashuke au wenye herufi zinazoanzia C, O, F, R.
Sayari hii ni ya kijani kibichi na wakati mwingine hugeuka wekundu, hupitia katika kila nyota siku ishirini na nane na kupitia katika kila Sayari kwa miezi sita. kwa maana ikikaa kwenye nyota yako mambo yanayokutokea yatakuwa yanahusiana na Sayari hii kama yalivyoainishwa hapa chini
Dua ya kusoma siku ya Jumatano ni ‘Yaa ghaniyu’ yaa adhwim.
Kafara ya Jumatano ni ‘Mchanga mwekundu unauusomea au kunuwia haja uitakayo au umwage mbele yako au umpige nayo adui yako na atapata matatizo.
Mafusho yake yanaitwa Kashuu Muhlib au ‘kachiri’ ambayo yako kama maua yanayokauka na rangi yake ni kahawia ‘Brown’
INAHUSIKA NA NINI?
Sayari hii ya Mercury-Attarid inahusika na mambo yanayohusiana na Adabu, Malezi mema, Mantiki, Kupata kitu, Fasihi ya lugha, Ufahamu, Uelewa, Elimu, Urafiki, Hila na kudanganya, Hesabu, Vitabu, Sanaa za aina zote, Ukatibu au Ukarani, Shule au Kumpeleka mtoto shule.
Vile vile inahusiana na mambo ya Nakshi, masuala ya Urembo, kuandaa majeshi, nidhamu na leo ni siku nzuri kuvaa nguo za hariri. Kwa ujumla ni Sayari ya mapato.
FANYA YAFUATAYO
Siku ya Jumatano ni siku nzuri ya kuwafukuza maadui au kuwapatanisha mke na mume, wapenzi au Marafiki waliogombana au kama wewe ni kiongozi wa Nchi ni siku nzuri kuanza kukusanya majeshi kwa ajili ya kupigana vita.
Siku ya leo unashauriwa kuwa ujihadhari kuvaa nguo mpya unaweza kupata balaa, vilevile unashauriwa usisafiri kwa sababu unaweza kupatwa na upepo mbaya.
Leo Jihadhari sana kufanya Biashara hasa kununua na kuuza, Leo ni siku nzuri kwa biashara ya nguo au udobi tu au biashara ya kufundisha watoto au wewe mwenyewe kuanza masomo ya aina yeyote.
HAJA UTAPATA AU HUPATI?
Jumatano ukiulizwa kama haja itapatikana, jibu kwamba kama ni mwanzo wa siku kuanzia Saa 12 hadi Saa 5 haja haipatikani.
Katikati ya siku kuanzia Saa 6 hadi Saa 9 haja au ushindi utapatikana kwa taabu na mashaka.
Jioni kuanzia Saa 9 hadi Saa 12 haja itapatikana kwa urahisi.
SUALA LA ANAEULIZA?
Mtu akikujia siku ya leo atakuwa anataka kujua juu ya kitu chenye kuundwa undwa, chenye thamani au ni kama pesa au kitabu au khatima au katibu mkuu au mjumbe au mhasibu.
Jumatano ukiulizwa kuhusu watu waliogombana au maadui waliokosana sema kwamba kati yao wawili hamna kheri wala shari. Mwambie kwamba kila mtu kati yao anamfikiria mwenzie ubaya na maovu, mwambie kwamba kati yao kuna fitina kubwa na hakuna maelewano wala muafaka.
Ukiulizwa kuhusu kilichopotea, sema kwamba kitu hicho hakipatikani mpaka zipite siku nyingi ndio kitaonekana.
Jumatano ukiulizwa juu ya mtu aliye mbali, sema kwamba mtu huyo atakuja hivi karibuni, sasa hivi au leo au wakati wa Magharibi au siku yeyote kabla ya Jumatano.
Mwambie kwamba yeye ni mzima na mali yake ni salama na hivi sasa yuko katika gari au ndege au meli anakuja tokea sehemu za Magharibi na anaongozana na mtu mashuhuri.
Pia mwambie kwamba kuna kitu kidogo alichopoteza kama Pesa au Mnyama au Gari au kipandio kuharibika na haitozidi siku tano au 10 atarejea.
Ukiulizwa kuhusu mwaka huu utakuwaje, mwambie kwamba mwanzoni na mwishoni mwaka utakuwa mbaya na vifo vitakuwa vingi vitakavyosababishwa na Subiani na atakufa msomi mkubwa wa mji huo.
KHABARI
Leo Jumatano Ukiulizwa juu ya khabari, sema kwamba khabari yeyote utakayopata leo ikiwa ni mbaya au nzuri au ikiwa inahusu Mwanaume au Mwanamke au yasiyokuwa hayo basi khabari hiyo ni kweli kabisa.
MAGONJWA
Jumatano Ukiulizwa juu ya Mgonjwa, sema kwamba huyo Mgonjwa, ugonjwa wake unatokana na upepo wenye kuweza kutibika. Mwambie kwamba ni ugonjwa wa kuchanganyika na katika kichwa chake kuna kitu kichafu.
Mwambie kwamba Mgonjwa huyo anaumwa mwili mzima na kuna kitu anahisi kinatembea kutoka kitovuni mpaka mgotini. Mgonjwa ana maumivu makali katika shingo yake na ugonjwa huu huwa unamrudia mara kwa mara.
Mwambie mashahiba au watu wake wana wasiwasi kwamba atakufa kwa sababu ya maradhi hayo.
Mwambie sababu ya maradhi hayo ni husda ya maadui zake na watu wengine ambao wanalitaja jina lake usiku na mchana.
Mwambie dawa yake ni yeye achinje hamani na aipike kwa samli ya Ng’ombe, aongeze kiini cha yai na sukari kidogo na haba moja ya kufuri mchanganyiko huo apewe mgonjwa ale atapata nafuu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
MWIZI (MUHUSIKA)
Jumatano Ukiulizwa juu ya (MUHUSIKA) Mwizi, sema kwamba ikiwa ni mwanzo wa siku Mwizi atakuwa ni mtu mwenye rangi ya kahawia, mng’avu, mwenye pua ndefu na =mwenye haya kidogo.
Mwambie kwamba (MUHUSIKA) Mwizi huyo ni msomi au mwenye kusomesha au msomaji ama yeye anasomesha watoto wa watu. Sema ni mtu mwenye umbo fupi na atakuwa mtu wa karibu yako mfano familia yako au rafiki yako au kipenzi chako au jirani yako. Mweleze huyo Mwizi anapenda kubeba vitabu au vitu kama hivyo.
Mweleze kitu kilichoibiwa kimetundikwa kwenye hewa au kimezikwa ardhini lakini kitapatikana.
Mwambie ikiwa ni mwisho wa siku au jioni basi atakuwa mtu mwenye rangi nyekundu mwenye umbo fupi na ana nywele nzuri. Mweleze kwamba kijana huyo ni msomi au ni mwenye kuhifadhi Koran au Biblia.
Sema kwamba kitu alichokiiba amebadilishana na kitu kingine. Mweleze huyo aliyebadilishana nae ni mtu mzuri, tajiri na ni kijana wa kiume wa hapo mjini.
Mwambie kitu kilichoibiwa hakitaonekana ila kwa taabu na shida.
SAFARI
]Jumatano Ukiulizwa juu ya Safari, sema kwamba kama ni safari ya nchi kavu basi itatimia, lakini ikiwa ni safari ya baharini au nchi za nje itabidi ungoje kwa muda wa wiki mbili au miezi miwili au miaka miwili.
Endelea kumweleza kwamba kuna uzito na taabu hasa kwa vile hivi sasa unashirikiana katika safari hiyo na mtu mmoja ambaye ni Muongo au kuna mtu mnaushirika juu ya jambo au kuchanganyika pamoja.
Mwambie kwamba ajihadhari naye kwani mtu huyo ni mwongo na atakushughulisha katika mambo mengi ya uongo kuhusu safari hiyo.
Mweleze kwamba akisafiri baharini bila kungoja hizo wiki mbili atapigwa na upepo mkali na meli au chombo atakachosafiria kitazama au kupinduka lakini yeye atanusurika.
Mwambie kwamba habari hizo inahusu safari inayoanzia mwanzo wa siku lakini kama akisafiri katikati ya siku kuna mawili yatatokea, kuna uzito na kuna wepesi.
Mwambie mwanzo wa siku ni kwa safari za nchi kavu tu, kwa safari za baharini lazima asubiri wiki moja au mwezi mmoja au miaka miwili.
NDOA
Leo Jumatano Ukiulizwa juu ya Ndoa sema kwamba ndoa itawezekana tu ikiwa ni kwa mjane ambae si mtu wa kwenu au ifungwe mbali na hapo.
Sema kwamba Mwanamke anayetaka kuolewa hana mapenzi ya dhati kama alivyo mwanamme na lazima ifanyike dawa kurekebisha mapenzi ya Mwanamke.
Mweleze kwamba mazungumzo ya ndoa yapo na yatakuwepo lakini kuna mtu wa nje ambaye anayefanya mipango hiyo ya Ndoa mpaka akirudi ndio ndoa itatimia.
Kwa kawaida Jumatano ndoa huwa haitimii kwa sababu mwanamke huwa anapata ushawishi kutoka kwa mwanamme mwingine ambaye hayupo hapo, yupo mbali. Ukitaka ndoa muone mwalimu akufanyie azima ndipo ndoa itatimia inshallah.
MIMBA
Leo Jumatano Ukiulizwa juu ya Mimba sema kwamba mzazi atazaa watoto wawili (Mapacha), Mke na Mume. Mweleze kwamba mmoja ya watoto hao ana damu ya Jini na mwingine ana damu ya Kibinaadamu.
Mweleze kwamba mtoto wa kiume atakuwa mtambuzi na mwenye akili nyingi, msomi na atakuwa na umri mrefu na utajiri mwingi na mtoto huyo atapendwa na wengi kwao na nje ya nchi.
NANI MSHINDI
Ukiulizwa leo Jumatano nani atashinda sema kwamba kwa wanaoshindana matokeo ni sare hakuna mshindi wala mshindwa.
Sema kwamba kila mmoja amefanya njama mbaya kwa mwingine na kuna fitina mbaya kati yao na mwisho hawatakubaliana wala kusikilizana.
No comments:
Post a Comment